Tuesday, January 10, 2012

Mapenzi na amani katika ndoa baada ya kuwa na watoto

YAPO mambo mbalimbali ya kuzingatia baada ya wanandoa kupata watoto na baadhi yao wakawa wanasoma au wanahitaji malezi nyumbani.

Kwanza, ni muhimu kuwa na mipango na ratiba za shughuli zote za nyumbani kwa upande wa mama na wasaidizi wake. Nyumba yenye upendo na amani aghalabu mambo yake huenda kwa kiasi na wakati maalum na hayaendi kwa kubahatisha.

Mathalani, kwa watoto wanaokwenda shule, nguo zao budi kufuliwa na kupigwa pasi zikawa tayari leo, kama shule ni kesho. Aidha, mahitaji mbalimbali ya wanaokwenda shule huwa yameainishwa na kuandaliwa kabla ya siku yanayotakiwa.

Watoto kama ni wa shule ya siku (wanakwenda na kurudi kula mchana), lazima wakute chakula kiko tayari na sio kiwe kinaandaliwa baada ya watoto kurudi toka shule.

Aidha, masula ya kununua vitu vya matumizi ya nyumbani, usafi na utunzaji nyumba kwa ujumla ni lazima vifate ratiba au utaratibu ambao hauwaingilii wanafamilia akiwemo baba katika shughuli zake nyingine hapo nyumbani.

Na masuala haya ni ya familia. Sio masual aya sanaa na kuigiza. Hakuna kitu kinachoudhi kama wanafamilia kuwa wasafi na wastaarabu pale tu wageni wanapotarajiwa kuja. Usafi na ustaarabu lazima uwe ni sehemu ya kila siku ya familia ya kiungwana.

Athari za kuoa au kuolewa na mtu wa dini nyingine

MAPENZI kati ya watu wenye dini tofauti huweza kuwa makali kuliko hata ya wale wa dini moja. Lakini hakuna kitu kibaya na kichungu kama kukosa upendo na maelewano baada ya kuona na kuishi kama watu wa dini mbili tofuati.

Shetani wa kila aina na majaribu ya kila sampuli huvamia nyumba yenu na mkawa ni watu wanaoishi bila upendo, maelewano wala masikilizano.

Busara na hekima za watu wa kale bado ni muhimu, kwa kuwa yaliyo mengi wamekwishayaona. Usidanganye na lewalewa la pendo la hivi sasa, lakini ukaja kuishi kwenye maisha ya masikitiko na kujuta kwa miaka yote inayobakia katika maisha yako. Kuamua ni kuchagua. Na uamuzi ni wako.

Saturday, September 17, 2011

Nichague vipi wa kuoa ?

YAPO mengi kuhusu jinsi ya kuchagua mke wa kuoa. Leo tunazungumzia kuhusu tu akili za watoto watarajiwa na mnasaba wa fungate.

Aidha baba anaweza akawa na akili (intelligence) au kinyume cha hivyo. Kwa kuzingatia kwamba watoto wengi hushabihiana na mama si vizuri kumuoa mwanamke ambaye darasani anashika mkia. Na hususan pale unapokuwa na wasiwasi kwamba watoto watamfuata mama zaidi kuliko wewe kihulka na kitabia.

Ukigundua fika kwamba watoto lazima watakuwa kama wewe basi unaweza kuidharau amri hii. Kama sivyo, ni hatari kwako kwa sababu watoto watakaozaliwa watakuwa na akili pungufu ya hata hizo ambazo wewe usiye na akili huna kabisa.

Ni katika muktadha huu ndio maana matajiri,wanasayansi wenye akili za kupindukia, maprofesa, marais, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao wanaoa au kuolewa na watu wenye akili duni wanazaa watoto bomu zaidi.

Matokeo yake mama au baba anaanza kumsukuma na kumburuza mtoto aisyekuwa na akili aanze kuwa na akili kama vile mtoto wa fulani. Wakati mwenziwe aliangala kwanza kisha akaoa mtu mwenye akili ili azae watoto wenye akili. Ukweli ni kwamba kama zilivyo mbegu ukipanda mbegu mbovu kwenye shamba bovu unazaa mbegu mbovu au mimea mbilikimo isiyokuwa na isiyoonesha kwamba ni mmea gani tarajiwa.

Katika nchi ambazo wanasiasa na mangimeza wa serikali wanashindana kuwarithisha watoto wao 'vihiyo wenye digrii feki' ukubwa, hili husababisha nchi kuwa na viongozi dhaifu na ambao majibu yao kwa kila kitu si nguvu ya hoja bali hoja ya nguvu kama tunavyoona Syria, Gabon, Cameroun, Ethiopia, Eritrea na kwingineko.

Sikatai yapo majaliwa. Na kwamba Mwenyezi Mungu huweza kuwajalia wazazi wawili wasio na akili mtoto mwenye akili kama mchwa. Lakini lazima katika historia ya watu hao utakuta kuna babu au bibi alikuwa jiniasi wa aina fulani. Kwa hiyo ni lazima kuchunguza historia ya wenzi wetu vyema kabla ya kuamua kuingia kwenye kifungo cha ndoa.

Ninaamini, hakuna anayependa mwanae 'mjinga' kila siku kuambiwa angalia akili zako kama za mama au baba yako. Ndio maana tunapaswa kufanya biashara ngumu ya kuchagua kati ya figa, sura, tabia na akili. Na wengi wanaamini bora kuzaa mtoto asiyekuwa na figa wala sura lakini mwenye akili nyingi na tabia nzuri au sio?

Tuesday, December 1, 2009

Kwanini watoto wa Marais hutaka urais

HAPA Afrika wanasiasa kwa makusudi wameifanya siasa ionekane ni kazi bora na ya heshima zaidi kuliko kazi nyingine. Kutokana na hilo basi kila mtu kuanzia askari hadi Zuzu wote wanataka kuwa wanasiasa.

Mtu ataacha kazi yenye faida kubwa kwa binadamu wengine kama vile daktari na kwenda kwenye siasa. Mwalimu ataacha kufundisha na kujenga kizazi kipya na kwenda kudanganya watu kwa kuwa tu jambo hilo lina maslahi zaidi kuliko ualimu. Na viongozi wa dini inaelekea nao wameshagundua hili. Karibuni tutaanza kuona wakivua majoho na kuelekea kwenye vijiwe vya siasa.

Maelezo hayo kwa ufupi yanatosha kutoa picha kuonesha ni kwanini hata watoto wa Marais wanakuwa na wakati mgumu wa kuchagua kazi nyingine. Hii ni kwa kuwa kazi wanayoiona inalipa ni hiyo moja tu ya urais. Halitakuwa jambo la kushangaza kwa hiyo watoto wa Omar Bongo, Ben Ali, Museveni, Mubarak na kadhalika wakiachiwa kuendeleza usultani mpya katika Afrika. Sio jambo la kushangaza kwa kuwa jamii, mazingira na wanasiasa wetu hawakutaka kuwapa fursa watoto hao wa marais na wa wengine ya kuona kwamba kuna kazi nyingine bora zaidi ya urais.

Afrika na watu wake watabaki kutamani kuona siku ambayo uanasiasa Afrika unachukua nafasi inayostahili, yaani, nyuma ya kazi na majukumu mengine ya maana zaidi. Na hadi kufikia hapo Afrika itaendelea kupiga maktaimu kimaendeleo.

Malezi na tabia ukubwani

MALEZI ya mtoto huamua kwa kiasi kikubwa mtoto atakuwa na tabia gani. Kwa mfano, mtoto ambaye mama yake hajali yuko wapi saa zote hatoacha kuja kuwa mzururaji. Na mtoto nayeomba hela kutoka kwa watu asiowajua hatoacha na yeye kuja kuwa mtu asiye na aibu kama ombaomba.

Aidha, mtoto anayeruhusiwa kwenda anakotaka, aghalabu, hukutana na mengi yasiyo ya kawaida. Ndivyo inavyotokea kwa watoto wanaokwenda nyumba zenye wabwia unga ana hatari ya kuonjeshwa huo unga. Na kama tunavyojua mtoto akishauonja atataka tena na tena. Kuanzia hapo utakuwa huna mtoto.

Hali kadhalika mtoto wa kike anayeachiwa kujihusisha na changudoa ni vigumu yeye kuwa salama. Atakuwa anayaona hayo anayoyaona na kwa kuwa yeye ni binadamu atataka kujaribu. Akijaribu na akiona utamu basi utakuwa tena umekwishampoteza mtoto. Sidanganyiki bora zaidi ni ile ya kumlea mtoto awe mbali na mambo machafu na ya hatari.