Saturday, September 17, 2011

Nichague vipi wa kuoa ?

YAPO mengi kuhusu jinsi ya kuchagua mke wa kuoa. Leo tunazungumzia kuhusu tu akili za watoto watarajiwa na mnasaba wa fungate.

Aidha baba anaweza akawa na akili (intelligence) au kinyume cha hivyo. Kwa kuzingatia kwamba watoto wengi hushabihiana na mama si vizuri kumuoa mwanamke ambaye darasani anashika mkia. Na hususan pale unapokuwa na wasiwasi kwamba watoto watamfuata mama zaidi kuliko wewe kihulka na kitabia.

Ukigundua fika kwamba watoto lazima watakuwa kama wewe basi unaweza kuidharau amri hii. Kama sivyo, ni hatari kwako kwa sababu watoto watakaozaliwa watakuwa na akili pungufu ya hata hizo ambazo wewe usiye na akili huna kabisa.

Ni katika muktadha huu ndio maana matajiri,wanasayansi wenye akili za kupindukia, maprofesa, marais, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao wanaoa au kuolewa na watu wenye akili duni wanazaa watoto bomu zaidi.

Matokeo yake mama au baba anaanza kumsukuma na kumburuza mtoto aisyekuwa na akili aanze kuwa na akili kama vile mtoto wa fulani. Wakati mwenziwe aliangala kwanza kisha akaoa mtu mwenye akili ili azae watoto wenye akili. Ukweli ni kwamba kama zilivyo mbegu ukipanda mbegu mbovu kwenye shamba bovu unazaa mbegu mbovu au mimea mbilikimo isiyokuwa na isiyoonesha kwamba ni mmea gani tarajiwa.

Katika nchi ambazo wanasiasa na mangimeza wa serikali wanashindana kuwarithisha watoto wao 'vihiyo wenye digrii feki' ukubwa, hili husababisha nchi kuwa na viongozi dhaifu na ambao majibu yao kwa kila kitu si nguvu ya hoja bali hoja ya nguvu kama tunavyoona Syria, Gabon, Cameroun, Ethiopia, Eritrea na kwingineko.

Sikatai yapo majaliwa. Na kwamba Mwenyezi Mungu huweza kuwajalia wazazi wawili wasio na akili mtoto mwenye akili kama mchwa. Lakini lazima katika historia ya watu hao utakuta kuna babu au bibi alikuwa jiniasi wa aina fulani. Kwa hiyo ni lazima kuchunguza historia ya wenzi wetu vyema kabla ya kuamua kuingia kwenye kifungo cha ndoa.

Ninaamini, hakuna anayependa mwanae 'mjinga' kila siku kuambiwa angalia akili zako kama za mama au baba yako. Ndio maana tunapaswa kufanya biashara ngumu ya kuchagua kati ya figa, sura, tabia na akili. Na wengi wanaamini bora kuzaa mtoto asiyekuwa na figa wala sura lakini mwenye akili nyingi na tabia nzuri au sio?

No comments:

Post a Comment