Tuesday, December 1, 2009

Kwanini watoto wa Marais hutaka urais

HAPA Afrika wanasiasa kwa makusudi wameifanya siasa ionekane ni kazi bora na ya heshima zaidi kuliko kazi nyingine. Kutokana na hilo basi kila mtu kuanzia askari hadi Zuzu wote wanataka kuwa wanasiasa.

Mtu ataacha kazi yenye faida kubwa kwa binadamu wengine kama vile daktari na kwenda kwenye siasa. Mwalimu ataacha kufundisha na kujenga kizazi kipya na kwenda kudanganya watu kwa kuwa tu jambo hilo lina maslahi zaidi kuliko ualimu. Na viongozi wa dini inaelekea nao wameshagundua hili. Karibuni tutaanza kuona wakivua majoho na kuelekea kwenye vijiwe vya siasa.

Maelezo hayo kwa ufupi yanatosha kutoa picha kuonesha ni kwanini hata watoto wa Marais wanakuwa na wakati mgumu wa kuchagua kazi nyingine. Hii ni kwa kuwa kazi wanayoiona inalipa ni hiyo moja tu ya urais. Halitakuwa jambo la kushangaza kwa hiyo watoto wa Omar Bongo, Ben Ali, Museveni, Mubarak na kadhalika wakiachiwa kuendeleza usultani mpya katika Afrika. Sio jambo la kushangaza kwa kuwa jamii, mazingira na wanasiasa wetu hawakutaka kuwapa fursa watoto hao wa marais na wa wengine ya kuona kwamba kuna kazi nyingine bora zaidi ya urais.

Afrika na watu wake watabaki kutamani kuona siku ambayo uanasiasa Afrika unachukua nafasi inayostahili, yaani, nyuma ya kazi na majukumu mengine ya maana zaidi. Na hadi kufikia hapo Afrika itaendelea kupiga maktaimu kimaendeleo.

Malezi na tabia ukubwani

MALEZI ya mtoto huamua kwa kiasi kikubwa mtoto atakuwa na tabia gani. Kwa mfano, mtoto ambaye mama yake hajali yuko wapi saa zote hatoacha kuja kuwa mzururaji. Na mtoto nayeomba hela kutoka kwa watu asiowajua hatoacha na yeye kuja kuwa mtu asiye na aibu kama ombaomba.

Aidha, mtoto anayeruhusiwa kwenda anakotaka, aghalabu, hukutana na mengi yasiyo ya kawaida. Ndivyo inavyotokea kwa watoto wanaokwenda nyumba zenye wabwia unga ana hatari ya kuonjeshwa huo unga. Na kama tunavyojua mtoto akishauonja atataka tena na tena. Kuanzia hapo utakuwa huna mtoto.

Hali kadhalika mtoto wa kike anayeachiwa kujihusisha na changudoa ni vigumu yeye kuwa salama. Atakuwa anayaona hayo anayoyaona na kwa kuwa yeye ni binadamu atataka kujaribu. Akijaribu na akiona utamu basi utakuwa tena umekwishampoteza mtoto. Sidanganyiki bora zaidi ni ile ya kumlea mtoto awe mbali na mambo machafu na ya hatari.